WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Mpigakura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Waziri Mkuu ambaye alifuatana na mkewe Mama Mary Majaliwa, alijiandikisha leo (Jumamosi, Oktoba 19, 2024) kwenye shule ya msingi Nandagala iliyopo kitongoji cha Nanguruwe, Kata ya Nandagala, wilayani Ruangwa akiwa na baadhi ya wanakijiji wenzake ambao walifika kituoni hapo.
Mapema, akitoa taarifa ya uandikishaji, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ruangwa, Frank Chonya alisema wilaya ya Ruangwa ina tarafa tatu, kata 22, vijiji 90 na vitongoji 435 ambavyo vitahusika kwenye uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Vijiji.
Alisema wilaya hiyo imekadiria kuandikisha wakazi 123,803 ambapo kati yao 60,188 ni wanaume na 63,615 ni wanawake. “Hadi kufikia tarehe 18 Oktoba, 2024, tumefanikiwa kuandikisha jumla ya watu 103,468 ambapo kati yao wanaume ni 47,664 na wanawake ni 55,804.”
Alisema zoezi hilo la uandikishaji litaendelea hadi kesho tarehe 20 Oktoba, 2024 saa 12 jioni.
Akizungumza na wananchi waliokuwepo kwenye kituo hicho, Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, aliwashukuru viongozi wa Serikali za Vijiji wa Kata ya Nandagala kwa kuhamasisha watu wajitokeze kujiandikisha na kuifanya kata hiyo iwe ya kwanza kwa uandikishaji katika jimbo hilo.
“Kazi ya uandikishaji inaendelea nchi nzima na mwisho wa uandikishaji ni kesho. Tuwahimize wengine ambao bado hawajajiandikisha, nao pia waje kujiandikisha,” alisema.