Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Feb 27, 2023 amepiga marufuku vifungashio visivyo rasmi vya Mafuta ya mawese maarufu kama (Bidoo) Mkoani Kigoma ambavyo vimekuwa vikihifadhi mpaka lita 25 za Mafuta huku mkulima akilipwa bei ya lita 20.
Majaliwa ametoa agizo hilo alipotembelea viwanda vya kuchakata Mchikichi katika eneo la Sido Kigoma ambapo amemuagiza mkuu wa mkoa wa Kigoma kukamata vifungashio vyote ambavyo vimekuwa vikimnyonya Mkulima na mfanyabishara wa mawese.
“Bado hatujafikia hatua hiyo kwa sababu ya kuwa mnyonge kwa mnunuzi kwa sababu mahitaji ya mafuta ya mawese ni makubwa kuliko mahitaji, mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji wetu, kataa bidoo ukiona mtu analeta bidoo nenda kwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa”- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa pita kwenye masoko yote kagua kamata bidoo zote na usione huruma na mtu wa bidoo na wanunuzi mmenisikia na hizo bidoo zenu marufuku kuanzia sasa”- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Wanunuzi wa mafuta ya mawese wamekuwa wakitumia vifungashio vya madumu kwa jina maarufu hapa Mkoani Kigoma Bidoo kwa kufanya udanganyifu wa kuweka kwanza maji ya moto ambayo hutanua dumu hilo na kuongeza ujazo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kupokea kero hiyo anaeleza jitihada ambazo serikali inafanya kuliongezea thamani zao na mafuta hazipaswi kukwamishwa na watu wachache kwa faida.