Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo ametoa rai kwa vijana na wanawake kote nchini kuchangamkia programu ya uwezeshaji kiuchumi iliyozinduliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA (ICTC), na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuboresha bunifu zao za kibiashara.

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo wakati wa Semina ya Uwekezaji na Fedha ya Benki ya CRDB maarufu kama “CRDB Bank Uwekezaji Day” iliyoenda sambamba na uzinduzi wa taasisi ya hisani ya CRDB Bank Foundation, pamoja na programu hiyo ya iMBEJU ambayo inalenga kutoa mafunzo, ushauri, na mitaji wezeshi kwa vijana na wanawake.

Waziri Mkuu amesema programu hiyo imekuja kutoa suluhisho kamili kwa biashara changa za vijana na wanawake nchini kwa kuzijengea uwezo wa kujiendesha hususani kupitia mafunzo ya kimkakati ambayo yamepangwa kutolewa kwa kushirikiana na ICTC, COSTECH, pamoja na wadau wengine katika programu za uwezeshaji wanawake kupitia vikundi.

“Ukweli ni kuwa tatizo la kushindwa kuendelea kwa biashara changa si kukosekana kwa mitaji. Mitaji ipo na taasisi zetu za fedha zipo tayari kufadhili, lakini hatari ya uchechefu ni kubwa kwani biashara changa nyingi zimekuwa zikishindwa kujisimamia. Niwashukuru Benki ya CRDB kwa kuliona hili na kuambatanisha programu ya iMBEJU na ushauri na mafunzo,” alisema.

Waziri Mkuu aliwataka vijana na wanawake kutumia vizuri mitaji watakayopewa kwa kuwekeza katika maeneo waliyoyaainisha kupitia mipango yao ya biashara, huku akiwasisitiza kuwa waaminifu. Alizitaka pia taasisi za Serikali kutoa fursa kwa vijana waliokuja na bunifu zinazoweza kutatua changamoto za jamii, akitolea mfano wa vijana waliobuni mfumo wa kuongoza magari barabarani kupewa fursa na Wizara ya Ujenzi.

Waziri Mkuu aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuja na programu hiyo, na kusema inaendana na dira ya serikali ya kuchochea ubunifu kwa vijana na wanawake ili kutengeneza ajira, na kuchochea maendeleo nchini. Waziri Mkuu aliwahakikishia vijana kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kufanikisha bunifu zao zinakuwa na tija kwao na kwa jamii kwa ujumla.