WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya ahakikishe mkandarasi anayejenga mabweni, madarasa na vyoo katika shule ya sekondari Mandawa awe ameanza kazi ifikapo Oktoba 24, mwaka huu.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo pamoja na viongozi wa Wilaya hiyo, leo (Jumatatu, Oktoba 21, 2024) mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeamua kuipandisha hadhi shule hiyo kwa kuamua kuifanya iwe na madarasa ya kidato cha tano na sita.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, yupo wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku nne, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa sh. milioni 545 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matatu, madarasa sita na matundu ya vyoo 12 katika shule hiyo, iliyopo kata ya Mandawa, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amekemea tabia ya watumishi kupokea fedha za miradi na kukaa nazo huku wakifanya vikao bila kufikia maamuzi yanayosaidia kuanza kwa utekelezaji wa miradi husika.
“Mmesaini mkataba Oktoba 8, mwaka huu, lakini mpaka sasa hakuna kazi yoyote iliyofanyika, hivi kweli tutamaliza majengo haya kwa wakati? Msingi wa bweni upo wapi? Tunataka ifikapo Desemba mwaka huu, majengo yawe yamekamilika ili Februari, 2025 tuweze kuisajili,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kuwa msisitizo wa Serikali ni kuona miradi yote inayoletewa fedha inakamilika na inaanza kutumika. “Wananchi wanapoona mradi unajengwa, wanataka kuona mradi huo unakwenda kwa haraka na kwa ubora ili ulete matokeo pale unapoanza kutumika.”
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata za Mandawa, Namichiga na Matambarale, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kazi kubwa inaendelea kufanyika katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na barabara.
“Leo katika wilaya hii vijiji vyote tumemaliza kuweka umeme na na sasa tunakwenda katika vitongoji. Tumemaliza kujenga shule za msingi, huko hatuna shida. Kwa upande wa sekondari, tumepiga hatua kubwa, kwani mwaka 2010 nilipoingia madarakani tulikuwa na shule tatu tu za sekondari, lakini leo 2024 tuna shule 30 za sekondari, lengo ni kuona watoto wa Ruangwa wanapata elimu mahali walipo.”
Akizungumzia kuhusu miundombinu ya barabara, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa kuna mtandao wa lami wa kilomita 24 Ruangwa mjini. “Pia tuna mpango wa kujenga kilomita 100 za barabara za vijijini kuelekea kwenye maeneo ya uzalishaji, ili kuongeza urahisi wa kufikisha mazao sokoni; zote hizi tunaziweka lami.”
Kwa ujumla, Waziri Mkuu amewaomba wakazi wa kata hizo waendelee kuwa watulivu na waendelee kuiamini Serikali yao.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Kaka Mkuu wa shule ya sekondari Mandawa, Saidi Mohammed Mkowola ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, matundu vya vyoo, vyumba vya madarasa pamoja na ujenzi wa maabara ya kemia na bailojia na ununuzi wa vifaa vingi vya maabara.