Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Urusi imeahidi kushirikiana na Afrika kuboresha uchumi ikiwemo Tanzania.
“Mwelekeo wa mkutano wa leo ilikuwa ni kuona namna gani tunaweza kuboresha uchumi wa nchi za Afrika kwa pamoja na Urusi, wao wametoa mwelekeo wa namna ambavyo wataweza kushirikiana na Nchi za Afrika kuboresha uchumi wa kila Nchi na sisi tumeeleza mkakati wa kiuchumi kwenye Nchi yetu ambao Rais Putin ameuridhia”
Majaliwa amesema hayo baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi ambako amemwajilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkutano huo umefanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, Jiji i St. Petersburg, Urusi.
Waziri Mkuu amesema Tanzania itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa lengo la kuboresha uchumi na biashara kwa kutumia rasilmali zake ikiwemo madini, maliasili na kilimo hasa upatikanaji wa mbolea. “Tumesisitiza pia matumizi ya nishati mbadala kama njia muhimu ya kuwawezesha wananchi wa vijijini ili nao wamudu kutumia nishati mbadala kukuza uchumi wao”