Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametembelea na kukagua ujenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mwanza, iliyopo wilaya ya Misungwi, kijiji cha Nyang’omango. Ujenzi wa kampasi hiyo ulianza Januari 22, 2022, na sasa uko asilimia 99 ukiwa na gharama ya zaidi ya shilingi bilioni saba.
Haya yalibainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo, wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo
Katika hotuba yake, Prof. Pallangyo ameeleza kuwa kampasi hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza fursa za kielimu kwa vijana wa eneo hilo na nchi kwa ujumla. Ameongeza kuwa ujenzi umezingatia viwango vya kimataifa ili kutoa mazingira bora ya kujifunzia.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyang’omango Peter Deus ametumia fursa hiyo kueleza changamoto zinazowakabili wananchi, hususan tatizo la maji. Ambapo amesema ingawa wanafurahia uwepo wa miundombinu ya TIA kijijini hapo, wanahitaji msaada zaidi katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.
Dkt. Mwigulu, akijibu changamoto hiyo, alisema tayari serikali imetenga fedha na imetoa hundi kwa mkandarasi kuendelea na utekelezaji wa mradi wa maji. Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wananchi wa Misungwi kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa haraka.