Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufikisha umeme kwenye minara inayojengwa ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji ikiwamo kutumia majenereta.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara inayojengwa na kampuni za simu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Amesema minara mingi inatumia jenereta, hivyo kuna umuhimu wa wakala huo kufikisha umeme ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Aidha, amewataka wananchi kutunza mnara huo uliojengwa katika Kijiji cha Kinua wiilayani hapa ambao umegharimu Sh. milioni 350 na ni mmoja kati ya minara 758 inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni lazima ilindwe.
Kuhusu umuhimu wa miundombinu hiyo ya huduma za mawasiliano, Waziri Nape ameeleza kuwa ina manufaa makubwa kwa wakazi wa vijijini kwani inawawezesha kuwasiliana kwa urahisi, kutumia huduma za kifedha, kupata huduma za afya na elimu.
Aidha, Waziri Nape amepongeza UCSAF kwa jitihada za kuhakikisha maeneo ambayo kampuni za simu hazikufanikiwa kupeleka minara kutokana na sababu za kibiashara yanafikiwa kwa kufadhili ujenzi wa minara.