Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi, ameeleza kuridhishwa na utendaji wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambao umeimarika kutokana na matumizi ya mifumo ya TEHAMA ambayo imeboresha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za usalama na afya nchini.
Ametoa kauli hiyo, alipotembelea banda la OSHA katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Saba Saba) yanayoendelea katika Viwanja vya Saba Saba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Temeke Jijini Dar es Salaam.
Waziri Ndejembi amesema mwelekeo wa serikali kwasasa ni kutoa huduma bora kwa wananchi katika hali ya urafiki zaidi pasipo kusukumana.
“Nafasi ya OSHA katika shughuli za uchumi wa nchi yetu ni muhimu sana kwani wajibu wao ni kuzuia ajali, magonjwa na vifo katika sehemu za uzalishaji. Hivyo, niwatake wajikite zaidi katika kujadiliana, kushauriana na kushawishi wadau kutekeleza sheria kwa hiari pasipo kushurutishwa. Nguvu inaweza kutumika kwa baadhi ya wadau ambao ni wakaidi tu,” ameeleza Ndejembi.
Aidha, ameitaka OSHA kuhakikisha kwamba mifumo yake ya kieletroniki inasomana na mifumo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili kuwawezesha wadau kufanya usajili katika dirisha moja na hivyo kuwaondolea usumbufu wa kuwa na mlolongo wa Taasisi wanazopaswa kufanya usajili.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema ushiriki wa OSHA katika maonesho hayo unalenga kuongeza uelewa wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa wadau wake ikiwemo kuonyesha jinsi OSHA inavyotekeleza majukumu yake pamoja na kutoa majawabu ya maswali ambayo wadau wamekuwa wakijiuliza kuhusu Taasisi hiyo yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya nchi.
“Ninawakaribisha wadau wetu na wananchi kwa ujumla kutembelea banda letu kwa ajili ya kuona uwekezaji mkubwa tulioufanya katika wataalam na vifaa vya kisasa vya kufanyia ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya. Uwekezaji huu unalenga kuunga mkono juhudu za Mheshimiwa Rais katika kuvutia biashara na uwekezaji kwani wawekezaji wanapenda kuwekeza katika nchi zenye mifumo bora na mojawapo ya mifumo inayoangaliwa ni mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) iliyopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambayo dhima yake kuu ni kulinda nguvukazi ya Taifa pamoja na mitaji ya wawekezaji kupitia ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mifumo ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali, magonjwa na vifo ambavyo husababishwa na vihatarishi vya usalama na afya mahali pa kazi.