Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amewataka Watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuongeza nguvu katika kusajili Waajiri na kuhakikisha kwamba Waajiri hao wanawasilisha michango ya Watumishi wao kwa wakati ili ije kuwasaidia Watumishi hao endapo watapata ajali, kuumia, ugonjwa au kifo kutokana na kazi zao.
Waziri Kikwete ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati wa kikao kazi baina yake na Watumishi wa WCF kwa lengo la kujadili na kuelekezana namna bora ya kuboresha utendaji kazi.
“Natambua kuwa hadi sasa WCF imesajili asilimia 93.7 ya Waajiri wote nchini lakini hiyo haitoshi na ninaitaka menejimenti ya ihakikishe kwamba Waajiri wote wanasajiliwa hadi kufiukia asilimia 100 na wanawasilisha michango yao kwa wakati. Na katika hili ninawahimiza watumishi wote muwajibike kutekeleza jambo hili, kwa kuwa ndio msingi mkuu utakaosaidia kulipa fidia kwa Wafanyakazi watakaopata ugonjwa, ajali au kufariki wakati wakitekeleza majukumu ya kazi.
Ridhiwani Kikwete pia ameiagiza Menejimenti ya WCF kuhakikisha inafanya uwekezaji katika maeneo yenye tija yatakayosaidia kuuongezea Mfuko uwezo wa kumudu kulipa fidia hususani katika maeneo ya hatifungani ambayo ni salama zaidi “Uwekezaji ni sehemu ya jukumu muhimu la WCF, na ili kuhakikisha eneo hili linakuwa na tija, basi mnapofikiria njia ya uwekezaji fikirieni maeneo yaliyo salama, ili kuuwezesha Mfuko kumudu jukumu lake la msingi ambalo ni kulipa fidia kwa Wafanyakazi wanaopata madhila kazini”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema kuwa Menejimenti imepokea maelekezo ya Waziri na kwamba Watumishi wataongeza kasi ya uwajibikaji ili kutekeleza maagizo hayo.