Waziri wa Afya Ummy Mwalimu @ummymwalimu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imempa ajira ya mkataba Mariam Mwakabungu (25) kama sehemu ya kuthamini mchango wake kwa kujitolea kuokoa maisha ya Watoto wachanga (Njiti) waliokimbiwa na Mama zao katika Hospitali ya Amana ambapo amekuwa akiwakumbatia ili wapate joto na kuongeza uzito.
Waziri Ummy amesema Rais Samia amefurahishwa sana na upendo wa Mariam na licha ya kumpa milioni 2 jana ameridhia Serikali impe Mariam ajira ya mkataba, kwakuwa hana vigezo vya kuajiriwa moja kwa moja kwa sasa lakini wamemshauri ajiendeleze kwanza kielimu ili apewe ajira ya kudumu hapo baadae.
“Kwakweli Mh. Rais ameguswa sana na moyo wa Mariam, Madaktari wanasema ana moyo wa kujitoa na anapenda kufanya hiyo kazi, ataingizwa katika utaratibu huo ili aweze kupata sifa, kwa sasa ana miaka 25 bado ana muda anaweza kusoma uuguzi ngazi ya astashahada akawa Muuguzi wa Watoto njiti”
@AyoTV_ ilipotaka kufahamu kama Serikali inao mpango wa kutoa ajira hizo kwa Watu wengi zaidi ili kuokoa maisha ya Watoto njiti, Waziri Ummy amesema kwa sasa wataanza na wale wenye moyo wa kujitolea kwanza ndipo wafikirie kuwaajiri “Tukipata Watu wenye moyo kama wa Mariam kwakweli tutakua tunawaajiri kwa mkataba, nikitoa wito watafurika wengi kwasababu wapo Watu mitaani hawana ajira”