Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Toto Afya Kadi haijafutwa ila kilichobadilika ni utaratibu wa kuwasajili ambapo utaratibu wa sasa ni kuwa Watoto wasajiliwe Shuleni kwa gharama ileile ya Tsh. 50,400 ili waingie wengi, wasio Wagonjwa na hivyo kuweza kuchangiana wachache watakaogua.
Akijibu hoja za Wadau mbalimbali kupitia mtandao wa X leo, Ummy amesema…. “Bima ni Sayansi, wakate wengi wachangiane wachache watakaougua, Toto Afya Kadi haijafutwa, kilichobadilika ni utaratibu wa kuwasajili, utaratibu wa sasa ni kuwa Watoto wasajiliwe Shuleni kwa gharama ileile ya Tsh. 50,400 ili waingie wengi, wasio Wagonjwa na hivyo kuweza kuchangiana wachache watakaogua”
“Kwa sasa Toto Afya Kadi wamesajiliwa Watoto laki 2 tu, tuhimizane Wazazi/Walezi kuwakatia Bima ya Afya Watoto wetu, naamini wakisajiliwa Watoto japo asilimia 10 tu (Milioni 3) kwa utaratibu huu basi tunaweza kuhakikisha ustahamilivu na uendelevu wa fao hili”
“Mwisho, Sera ya Watoto wa umri chini ya miaka mitano au Watu wasio na uwezo kupata msamaha bado haijafutwa, Hospitali zote za umma zinaendelea kuhudumia Watoto wa umri chini ya miaka mitano kupitia utaratibu wa misamaha”
“Nimeshaelekeza NHIF kutoa elimu zaidi kuhusu Watoto wanaokatiwa Bima ya Afya kwa hiari kuwa utaratibu wa sasa ni kuwa Watoto wasajiliwe kupitia Shuleni kwa gharama ile ile ya Tsh. 50,400 au kwa utaratibu wa kifurushi cha Familia, NHIF washirikiane na Kamati za Shule kutoa elimu hiii, nasi tuendelee kuhimizana na kuhamasishana kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa kila Mtu, tusisubiri hadi tuwe Wagonjwa ndio tukate bima”