Waziri wa Maji, Jumaa Aweso @jumaa_aweso amefika Kijiji cha Bitale Kata ya Mkongoro kilichopo Jimbo la Kigoma Kaskazini Wilayani Kigoma kuongea na Wananchi juu ya hatma ya mradi wa maji wa Mkongoro unaotekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Enabel ambapo amewapigitia goti Wananchi na kuwaomba radhi kutokana na kuchelewa kwa mradi huo.
Mradi huo ulitakiwa kukamilika tangu mwaka 2020 kwa utekelezaji wa kipindi cha miezi tisa na sasa ni mwaka wa tatu kazi haijakamilika na kutokana na hali hiyo Waziri amewataka Wafadhili wa mradi kuwa makini wakati wa mchakato wao wa manunuzi kwakuwa shida kubwa ni kupata Mkandarasi asiye na uwezo kwani changamoto kama hiyo imejitokeza pia katika Mradi wa Maji Kazuramimba Wilayani Uvinza.
Amesema hali kama hiyo inawachonganisha Wananchi na Serikali yao na kueneza chuki badala ya furaha na mafanikio kama yalivyo malengo ya ufadhili.
Akihitimisha mkutano na Wananchi waliokusanyika kwa wingi, ameelekeza Mkandarasi aitwaye Serengeti Limited kuondolewa katika utekelezaji wa mradi huo na kuiilekeza Wizara ya Maji kupitia RUWASA kukamilisha mradi huo katika kipindi cha miezi miwili Wananchi vijiji vyote saba kupata huduma ya maji akiwaelekeza kuanza hatua za dharura kwa kwa kuchimba kisima katika kijiji cha Bitale ambacho kina changamoto kubwa sana.