WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amewapongeza wawekezaji wazawa wa Kiwanda cha Mati Super Brands Limited kwa kulipa kodi stahiki za serikali na kutengeneza ajira kwa vijana hali inayochochea maendeleo ya Mkoa wa Manyara na taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho leo, Profesa mkumbo alisema wawekezaji hao wamelipa kodi ya shilingi bilioni 8 kwa mwaka 2024 na kuchangia maendeleo ya nchi.
“Rais Dr.Samia Suluhu Hassan anapambana kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania, na Mati Super Brands Limited imeajiri Watanzania 269,hilo ni jambo kubwa,” alisema Profesa Mkumbo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited, David Mulokozi alisema kuwa kiwanda hicho kina mchango katika jamii na kulipa kodi stahiki za serikali ikiwemo kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ushuru wa uzalishaji wa bidhaa, kodi ya mapato na kodi nyingine.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu tumekua tukilipa kodi ambapo mwaka 2022 tulilipa kodi ya shilingi bilioni 7, mwaka 2023 tulilipa kodi ya shilingi bilioni 7.9 , mwaka jana tulilipa kodi ya shilingi bilioni 8, na mwaka huu tunatarajia kulipa kodi ya zaidi ya shilingi bilioni 12,”alisema Mulokozi.