Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa mrengo mkali wa kulia wa Israel Itamar Ben-Gvir ametishia kujiondoa katika baraza la mawaziri la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu iwapo ataidhinisha makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas baada ya zaidi ya siku 460 za vita huko Gaza.
Ben-Gvir alikashifu makubaliano hayo siku ya Alhamisi jioni na kusema chama chake cha Otzma Yehudit chenye uzalendo wa hali ya juu – pia kinachojulikana kama Jewish Power Party – kitajiondoa serikalini ikiwa usitishaji mapigano utakamilika.
“Ikiwa mkataba huu usio na uwajibikaji utaidhinishwa na kutekelezwa, chama cha Jewish Power Party hakitakuwa sehemu ya serikali na kitauacha,” alisema.
Ben-Gvir pia alisema misaada ya kibinadamu na mafuta, umeme na maji lazima “ikomeshwe kabisa” kuingia katika eneo lenye vita la Palestina ili kulazimisha kuachiliwa kwa mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas.
“Hapo ndipo Hamas itawaachilia mateka wetu bila kuhatarisha usalama wa Israeli,” alisema.
Vile vile amemtaka Waziri mwenzake wa Fedha wa mrengo wa kulia wa Israel Bezalel Smotrich, Mkuu wa Chama cha Kidini cha Kizayuni na mkosoaji mwingine wa usitishaji vita, ajiondoe kwenye baraza la mawaziri iwapo usitishaji huo wa mapigano utaidhinishwa.