Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan atawezesha usafiri wa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati 250 kushiriki Maonesho ya 22 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika Jijini Kampala, Uganda kuanzia tarehe 8 hadi 18 mwezi Desemba 2022.
“’Kipindi cha miaka mingi, pamoja na mambo mengine, serikali imekua ikichangia usafiri wa mizigo ya Wajasiriamali kwenda kwenye maonesho. Kwa mwaka huu, Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Samia imepanga kuongeza mchango wake kwa kuwezesha usafiri wa basi la wajasiriamali kwenda na kurudi Uganda“
Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itatumia maonesho hayo kwa lengo la kuwawezesha vijana wajasiriamali wa Tanzania kutumia fursa hiyo kutafuta masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuwawezesha vijana kujiajiri na hivyo kukuza ajira na kuondoa umaskini.
Akiongea na Waandishi wa habari jijijini Dodoma, tarehe 21 Septemba, 2022, Mhe. Waziri Ndalichako amesema Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwezeshaji – Zanzibar, Wizara, Taasisi nyingine za Serikali na Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali imejipanga kukahikisha inaibua vijana wajasiriamali mahiri wakiwemo watu wenye ulemavu watakaoiwakilisha Tanzania katika maonesho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Vya Wajasiriamali Wadogo Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Joseph Rweyemamu, ameshukuru kwa jitihada ambazo serikali imeendelea kuzifanya katika kuhakikisha wanashiriki maonesho hayo. Aidha, ameahidi kutangaza bidhaa za Tanzania, Utalii pamoja na lugha ya kiswahili.