WCF yapongezwa kwa Ithibati ya ISO ya utoaji wa huduma kwa viwango vya kimataifa Katibu Mkuu – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu bi. Mary Maganga ameuagiza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuhakikisha inazingatia ubora wa huduma inazotoa kwa wananchi ili kuendana na ithibati ya utoaji wa huduma kwa viwango vya kimataifa, waliyopata.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya WCF kukabidhiwa Cheti cha Ithibati ya utoaji wa huduma bora kwa viwango vya kimataifa (ISO certification).
Akikabidhi cheti hicho kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, Bi. Maganga alisisitiza kuwa maboresho yanayofanywa na Mfuko huo yanapaswa kuzingatia mahitaji na matarajio ya wateja wake ili kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa haki yao ya fidia stahiki pale wanapopatwa na madhila yatokanayo na kazi zao.
“Kitu cha msingi ni kuhakikisha mnaendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma zenu. Nasisitiza mtumie ithibati hii mliyoipata kurahisisha taratibu za kuwasajili waajiri ili ikiwezekana waweze kujisajili wenyewe kwa hiari badala ya kulazimishwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria,” amesema Bi. Maganga.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa jitihada za kutoa elimu kwa wadau wake pamoja na kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali ili kuhakikisha huduma zake zinakidhi mahitaji ya wateja ni muhimu kuzingatiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amebainisha kuwa mafanikio waliyoyapata yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa wanaofanya katika matumizi ya mifumo ya Tehama. Ametoa rai kwa wadau wa Mfuko huo kutumia huduma za mtandao katika kupata huduma mbalimbali zitolewazo na WCF.
“Tumewekeza katika matumizi ya Tehama, ambapo kwa sasa takribani asilimia tisini ya huduma za Mfuko zinapatikana kwa njia ya mtandao ikiwemo usajili, kutoa taarifa ya madhila kutokana na kazi na kurekebisha taarifa za wafanyakazi. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaoishi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, aliyeelekeza kwamba mifumo ya taasisi zote ni vyema isomane ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Dkt. Mduma.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Viola Masako ameipongeza WCF kwa juhudi kubwa za utendaji hadi kufikia mafanikio hayo yanayoonesha nia thabiti ya Mfuko kuwajibika katika utoaji wa huduma kwa wateja wake kwa viwango vya kimataifa.
“TBS tunaipongeza WCF na tumeshukuru kwa jambo hili kwa sababu linatuongezea wigo wa kuisaidia Serikali yetu kutekeleza majukumu yake kwa wakati na pia kujipima namna ya kuboresha zaidi utoaji wa huduma zake kwa wananchi,” amesema Bi. Masako
WCF ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye jukumu la kutoa fidia kwa wafanyakazi pale wanapoumia, kuugua kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao na pale mfanyakazi anapofariki kutokana na kazi wategemezi wa familia yake hulipwa fidia na WCF.