Jumla ya wanafunzi 520 wa vyuo vitatu nchini wamenufaika na mradi wa ubunifu wa ‘Innoversity Project’ ambao unazisaidia taasisi za elimu ya juu nchini kuinua ubunifu na ujasiriamali zaidi ya taaluma na utafiti.
Mradi huo unalenga kuimarisha taasisi na nyenzo za elimu ya juu Tanzania, kusaidia safari ya ujasiriamali ya wanafunzi pamoja na kukuza ujasiriamali na ajira unafadhiliwa na ubalozi wa Ufaransa nchini unatekelezwa na kampuni ya Sahara Ventures wataalam wa biashara na kilimo pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH.)
Hayo yamebainika leo Jumatano Februari 8, 2022 katika ziara ya Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui katika ofisi za Sahara Ventures zilizopo jijini Dar es Salaam, alipofika kujua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa miaka miwili kwa gharama ya Euro 570,000 (sawa na Sh1.4 billion).
Akizungumza baada ya kupata maelezo ya maendeleo Balozi Hajlaoui amesema mradi huo wa uvumbuzi unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuvipa vyuo vikuu maarifa, zana na rasilimali za kukuza ubunifu, ujuzi wa kujiajiri na ujasiriamali na wanategemea matokeo chanya kwa kunufaisha Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
“Tunatekeleza mambo amabayo tulikubaliana na Rais Samia Suluhu Hassan alipokuja Paris Februari mwaka jana na kutembelea kituo cha uwezeshaji wafanyabiashara na wabunifu cha Station F Start Up facility,” amesema.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo uliyozinduliwa Mei mwaka jana Mkurugenzi wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike Amesema mradi unatekelezwa katika vyuo vikuu vitatu nchini ambavyo ni Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Afrika cha Nelson Mandela (Arusha), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Morogoro) na Chuo Kikuu cha Iringa.
Katika mchanganuo wa idadi kwa kila chuo na idadi ya wanafunzi wanufaika katika mabano; Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Morogoro (264), Chuo Kikuu cha Iringa (190), na ni Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Afrika cha Nelson Mandela (66).
“Mradi wa Innoversity umeshafikia wanafunzi zaidi ya 500, tumefanya kazi na walimu zaidi ya 38 wa vyuo na tayari kuna timu ya Tanzania imeenda Ufaransa na wa Ufaransa kuja hapa nchini kubadilishana utaalamu,” amesema