Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, limepokea magari mapya matatu ya kuzima moto kutoka kwa Shirika la Nyumbu lililopo Kibaha Mkoani Pwani ambalo lipo chini ya Jeshi la Wananchi na limekamilisha matengenezo ya magari hayo na yapo tayari kuanza kazi.
Magari hayo mapya yenye thamani ya zaidi ya Tsh. Bilioni 2.7 yenye uwezo wa kubeba maji lita 5,000/= na Foam lita 500 kwa kila gari, yamekabidhiwa kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini kutoka kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa.
Baada ya makabidhiano hayo Waziri Bashungwa amenukuliwa akisema “Uwekezaji wa Viwanda katika Sekta ya Ulinzi (Defence Industry) ni moja ya maono ya Mh. Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kujenga ustawi na kuimarisha Mashirika ya TATC Nyumbu na Mzinga ni kipaumbele kikubwa, nawapongeza TATC Nyumbu kwa uundaji wa magari ya zimamoto ambayo sasa yanaenda kutoa huduma kwa Wananchi kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji”
“Kuna shirika hili la Nyumbu na Mzinga yapo chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwahiyo zipo fursa za uwekezaji kwenye Wizara ya Ulinzi, walivyokuja Scania kuangalia engine wakaona utengenezaji wa bodi ya gari la zimamoto lililotengenezwa Nyumbu walishangaa sana wakaona kwa ubora huu hatuoni kwanini Tanzania iendelee kuagiza magari ya zimamoto wakati mnaweza kutengeneza hapa kwa viwango vya kimataifa na kupitiliza”
Kwa upande wake Kamishna Jenerali Masunga ametoa shukrani nyingi kwa Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuahidi kuyatunza Magari hayo na kuendelea kuwahudumia Wananchi katika huduma za Kuzima Moto na Uokoaji.