Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, litapunguza mpango wa mgawo wa chakula kwa wakimbizi walioko nchini Tanzania kuanzia mwezi ujao wa Juni.
Taarifa ya WFP imeeleza kuwa, zaidi ya wakimbizi 200, 000 nchini Tanzania watapewa tu nusu ya mgao wa chakula kuanzia mwezi ujao kutokana na ukosefu wa fedha za wafadhili.
Kupunguzwa kwa mgao wa chakula kwa mara ya pili nchini Tanzania katika miezi ya hivi karibuni, kunafuatia hatua kama hizo kote duniani huku shirika hilo la Umoja wa Mataifa likikabiliwa na ukata fedha taslimu na kupanda kwa bei ya chakula, hasa kutokana na vita vya Ukraine.
Mgao wa chakula kwa wakimbizi walioko nchini Tanzania ambao asilimia 70 wanatokea Burundi na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – umekuwa ukipungua taratibu tangu mwaka 2020, WFP ilisema katika taarifa.
Mwezi Machi, migao hii, iliyopangwa kukidhi kiwango cha chini kilichopendekezwa cha kilokalori 2,100 kwa kila mtu kwa siku, ulipunguzwa kutoka asilimia 80 ya kiwango hicho hadi asilimia 65.
Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa mamia ya wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchini humo tangu mwaka 2015 baada ya mzozo wa kisiasa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo hayati Pierre Nkurunziza.
WFP ilitangaza mwezi Machi kuwa mgao wa chakula pia utakatwa kwa wakimbizi nchini Burundi na Bangladesh, na kuomba ufadhili wa dharura ili kuepuka Yemen kupunguziwa zaidi.
Shirika hilo pia limepunguza mgao katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki katika miaka ya hivi karibuni ktokana na matatizo ya muda mrefu ya ufadhili, ikiwa pamoja na maeneo yaliyokumbwa na maafa ya Ethiopia, Sudan Kusini na Kenya.