Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya kuhusu uwezekano wa kusitishwa msaada wake wa chakula na lishe kwa watu milioni 1.4 walioathiriwa na mgogoro nchini Chad – ikiwa ni pamoja na wakimbizi wapya wa Sudan – kutokana na vikwazo vya fedha.
Haya yanajiri wakati mashirika ya misaada yakihangaika kujibu wimbi jipya la wakimbizi wanaokimbia janga la kibinadamu lisilofikirika linalotokea katika jimbo jirani la Darfur nchini Sudan huku kukiwa na ripoti za mauaji ya watu wengi, ubakaji na uharibifu mkubwa.
Pierre Honnorat, Mkurugenzi wa WFP nchini Chad, Jumanne akiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, N’djamena, nchini Chad, alionya kwamba, katika kipindi cha miezi sita tu ya vita nchini Sudan, wakimbizi wengi wamekimbilia Chad kama walivyovuka hadi katika miaka 20 iliyopita kuanzia kuzuka kwa mgogoro wa Darfur mwaka wa 2003. Amesema jumla ya idadi ya wakimbizi nchini Chad hivi sasa ni zaidi ya milioni moja, na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mojawapo ya idadi kubwa ya wakimbizi wanaokuwa kwa kasi zaidi katika bara zima la Afrika.
Aidha amesema, mgogoro wa Chad umesahaulika kwani macho ya ulimwengu yako kwenye dharura zingine, na kuongeza kwamba: “Inashangaza lakini watu wengi wa Darfur wamekimbilia Chad katika kipindi cha miezi sita iliyopita kuliko miaka 20 iliyopita.”