Shirika la haki za Binadamu la Amnesty International limeeleza kuwa Israel inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika ukanda wa Gaza kulingana na ripoti yake iliyotolewa mapema leo hii ambapo Shirika hilo limebainisha kuwa vitendo vya Israel vinavyosababisha maafa makubwa kwa Raia wa Kipalestima vinaonyesha nia ya kuangamiza Wapalestina kimwili huku Jumuiya ya kimataifa ikishindwa kuchukua hatua.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mashambulizi ya Israel yameharibu makazi na miundombinu ya Raia na kuzua changamoto za kibinadamu kama ukosefu wa chakula, maji na huduma za afya, Shirika la Amnesty pia limesema kuwa Israel imezuia misaada ya kibinadamu kufika Gaza hatua wanazosema ni sehemu ya mkakati wa kuwaletea Wapalestina mateso makubwa.
Tangu kuanza kwa mapigano baada ya shambulio la Hamas Oktoba 7, 2023, idadi ya vifo imefikia 44,532 upande wa Gaza huku zaidi ya asilimia 90 ya Wakazi wa eneo hilo wakifurushwa hivyo Shirika la Amnesty limelaani matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye msongamano wa Watu na imesisitiza kuwa hatua hizo hazina lengo la kijeshi pekee bali zinashiria mauaji ya makusudi.
Ripoti hiyo imejumuisha ushahidi wa matamko ya Maafisa wa Israel yanayodaiwa kuchochea uharibifu wa Gaza na kutaka kuifuta kabisa, aidha Amnesty imeonya kuwa Nchi zinazouza silaha kwa Israel zinahatarisha kushiriki katika mauaji hayo ya kimbari kisheria.
Hata hivyo Israel imekanusha madai haya ikisema kuwa operesheni zake ni za kijeshi dhidi ya kundi la Hamas ambalo linatumia Raia kama ngao za kibinadamu na Serikali ya Israel imeendelea kushikilia kuwa mashambulizi hayo yanahitajika kwa usalama wake wa Taifa.