Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni moja katika majimbo manane ya Msumbiji wameathirika na athari mbaya za kipindupindu, kimbunga Freddy na mafuriko yake, polio, janga la COVID-19 na janga la muda mrefu la kibinadamu kaskazini mwa nchi hiyo.
Severin von Xylander mwakilishi wa WHO, nchini Msumbiji amesema “Idadi ya waathirika ni kubwa. Zaidi ya watu milioni moja katika mikoa minane wanaathiriwa na kipindupindu, mafuriko na Kimbunga Freddy.”
Aidha afisa huyo wa Shirika la Afya Duniani amebainisha kuwa, kimbunga Freddy kiliharibu zaidi ya nyumba 132 na kusababisha watu 184,000 kuwa wakimbizi.
Uharibifu wa dhoruba hiyo kwa huduma za umma na miundombinu umekuwa wa kushangaza, WHO inasema, baada ya mafuriko mapema Februari yaliyosababishwa na mvua kubwa za msimu, na athari za kimbunga Freddy kupiga mara mbili tarehe 24 Februari na 11 Machi.
Tayari mamlaka za afya nchini Msumbiji zimetangaza kuwa, zimo mbioni kuanza kutoa chanjo dhidi ya kipindupindu katika mji wa Quelimane, ambao umeshuhudia uharibifu mkubwa kutokana na kimbunga Freddy.
Kimbunga Freddy kiliibuka mapema Februari kwenye pwani ya Australia na kimedumu hadi sasa na hivyo kutangazwa kuwa kimbunga kilichodumu kwa muda mrefu zaidi duniani. Kimbunga hicho kilivuka zaidi ya kilomita 8,000 kutoka mashariki hadi magharibi katika Bahari ya Hindi.
Kulingana na wataalamu ni kuwa, ongezeko la joto baharini huchangia kuongezeka kwa vimbunga. Dhoruba na vimbunga vya kitropiki hutokea mara kadhaa kwa mwaka kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi.