Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mkoa wa Tanga inawadai wamiliki wa maeneo makubwa kiasi cha Shilingi bilioni 3.4 ikiwa ni malimbikizo ya muda mrefu ya madeni yanayotokana na ardhi. Wamiliki hao, wengi wao wakiwa wafanyabiashara, wamepewa muda wa miezi sita kuhakikisha wanalipa madeni yao kikamilifu.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tanga, Tumaini Gwakisa, alitoa agizo hilo alipokutana na wadaiwa hao, akisisitiza kuwa kulipa madeni hayo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Alibainisha kuwa kutokulipa kwa wakati kunakwamisha juhudi za serikali katika kusimamia sekta ya ardhi na kuendeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wao, baadhi ya wamiliki wa maeneo hayo walieleza kuwa changamoto kubwa waliyoipitia ni ukosefu wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya ardhi na taratibu za ulipaji wa kodi na ada zinazohusiana na umiliki wa ardhi. Wameiomba serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu mara kwa mara ili kuwawezesha wananchi kuwa na uelewa sahihi na kuhakikisha wanakuwa na utamaduni wa kulipa kwa wakati bila kusubiri kusukumwa.
Wizara ya Ardhi inatarajia wamiliki hao kufuata maelekezo hayo na kuhakikisha kuwa madeni yote yanalipwa ndani ya muda uliopangwa ili kuepusha hatua zaidi za kisheria.