LEO Juni 06, 2023, Waziri wa sanaa, Utamaduni na michezo, Pindi Chana anawasilisha Bungeni Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ya Wizara hiyo.
“Wizara hii ni muhimu kwa nchi yetu, ambayo kwa maneno mengine naweza kusema ni Wizara yenye nguvu shawishi (soft power) ya nchi, kwa maana ya kuwa inawaleta wananchi wenye itikadi tofauti pamoja” – Waziri Pindi Chana
“Mheshimiwa Rais alinunua tiketi 2,000 wakati wa mchezo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam tarehe 28 Machi, 2023”– Waziri Pindi Chana
“Hivi karibuni tumeshuhudia akiridhia Kocha wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kulipwa mshahara na Serikali” – Waziri Pindi Chana #BajetiyaBurudani2023
“Rais amehamasisha timu za Yanga na Simba ambazo zimeshiriki mashindano ya kimataifa ngazi ya Afrika kwa kuwazawadia kila goli lililofungwa shilingi Milioni Tano (Sh. 5,000,000) katika hatua ya makundi” – Waziri Pindi Chana #BajetiyaBurudani2023
“Katika hatua ya fainali tumeshuhudia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiongeza dau kwa kuzawadia kila goli shilingi milioni ishirini”- Waziri Pindi Chana #BajetiyaBurudani2023
“Mchango wa Mhe: Rais ndiyo chachu ya mafanikio ya timu za Simba na Yanga katika mashindano haya. Hakika huyu ndiye mwanamichezo wa kweli na wa vitendo siyo wa maneno tu” – Waziri Pindi Chana #BajetiyaBurudani2023
“Naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa maendeleo ya nchi yetu. Pia, nimpongeze kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka miwili (2) ya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta zetu ambayo yametokana na uongozi wake ulio mahiri, wenye weledi, umakini na upeo mkubwa unaoendelea kulishamirisha Taifa letu ndani na nje ya nchi. Sisi na wadau wetu wote wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo tunamuahidi kuendelea kumpa ushirikiano, kuchapa kazi kwa bidii na kwa weledi ili kuendana na fikra, maono, na falsafa yake ya ìKazi Iendeleeî. Aidha, nitumie fursa hii kumuombea kiongozi wetu kwa Mwenyezi Mungu, awe na afya njema, Mungu aendelee kumpa hekima na busara katika kuiongoza nchi yetu‘ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani2023
‘Mchango wa Mheshimiwa Rais ndiyo chachu ya mafanikio ya timu za Simba na Yanga katika mashindano haya na kuiwezeshakufikia fainali kwa Timu ya Yanga na kama ambavyo Waswahili husema mwana hutazama uchogo wa mamaye, timu zinamwahidi kuendelea kuongeza jitihada. Hakika huyu ndiye mwanamichezo wa kweli na wa vitendo siyo wa maneno tu. Mheshimiwa Rais amekuwa akituunga mkono katika matukio na shughuli mbalimbali za Sekta zetu, ikiwemo Tamasha la Kimataifa la Michezo la Wanawake (Tanzanite International Women Sports Festival) na Mashindano ya Riadha kwa Wanawake ya Ladies First’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani2023
‘Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara ilikadiria kukusanya Shilingi Milioni Mia Tisa (Sh. 900,000,000) kutoka kwenye vyanzo viwili ambavyo ni mapato yatokanayo na viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru pamoja na Ada za mafunzo na mitihani kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya. Vyanzo vyote vinatoka Idara ya Maendeleo ya Michezo. Hadi kufika mwezi Aprili, 2023 Shilingi Milioni Mia Sita Themanini na Nane, Mia Nane Thelathini na Tisa Elfu, Mia Tano na Tisa (Sh. 688,839,509) sawa na asilimia 76.5 ya lengo zilikuwa zimekusanywa’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani2023
‘Miongoni mwa sababu za kutofikia lengo ni pamoja na kutokamilika kwa miundombinu ya kumbi zilizopo uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwemo vifaa; mwamko mdogo wa mashabiki kushabikia timu zilizopo nje ya kituo cha Dar es Salaam; na kutokuwasilishwa kwa wakati madai ya kodi ya pango katika eneo changamani la michezo Dar es Salaam’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Kwa upande wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, kiasi kilichokadiriwa kukusanywa ni Shilingi Bilioni Tano, Milioni Mia Tatu Tisini na Sita, Mia Nne Hamsini na Tano Elfu (Shilingi 5,396,455,000) ambapo shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Tisa Tisini na Nane, Mia Tatu Kumi na Tano Elfu, Mia Sita Kumi na Moja (Shilingi 2,998,315,611) sawa na asilimia 55.5 ya lengo zilikuwa zimekusanywa hadi kufikia mwezi Aprili, 2023’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani2023
‘Miongoni mwa sababu zilizochangia kutofikiwa malengo ni kutokana na wadau wengi wa filamu kufanya kazi zao bila ya kufuata utaratibu wa kisheria ikiwemo kukosa vibali na kuingiza filamu sokoni kabla ya kuhakikiwa; na kuchelewa kukusanywa na kugawanywa kwa mirabaha ya kazi za wabunifu. Fauka ya hayo, kwa upande wa vyuo, moja ya sababu ni wanavyuo kutokulipa ada kwa wakati kutokana na changamoto mbalimbali’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani2023