Shule ya Msingi Mazola, iliyopo katika kijiji cha Mazola, kata ya Doda, wilaya ya Mkinga, imepata afueni kubwa baada ya kukabidhiwa matundu ya vyoo 12 vilivyojengwa kwa msaada wa Shirika la World Vision kwa kushirikiana na serikali. Ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 86.4 na unalenga kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gibert Sylvester Kalima, akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, amepongeza Shirika la World Vision kwa kuwekeza katika mradi huo muhimu. Alibainisha kuwa vyoo hivyo vimezingatia mahitaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vyumba maalum kwa watoto wa kike na miundombinu rafiki kwa walemavu. Aliwahimiza walimu, wazazi, na wanafunzi kushirikiana kulinda na kudumisha vyoo hivyo kwa matumizi endelevu.
“Tumeshuhudia ujenzi wa viwango bora, na vyoo hivi vitaboresha hali ya usafi na kupunguza changamoto za kuchelewa darasani kwa wanafunzi waliokuwa wakilazimika kwenda nyumbani kwa ajili ya huduma za vyoo,” alisema Mhe. Kalima.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kushirikiana na serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha mchana mashuleni kwa lengo la kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi. Pia alikemea vikali unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, akitoa mwito wa ushirikiano wa kijamii katika kukomesha vitendo hivyo.
Kaimu Mratibu wa Mradi wa World Vision Mkinga Bi. Evodia Chija, alisema mradi huo utawanufaisha wanafunzi 131 wa shule hiyo, akisisitiza matumizi sahihi ya vyoo hivyo kwa maendeleo ya wanafunzi. Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Ndugu Omari Mashaka, aliahidi kuhakikisha miundombinu hiyo inadumishwa kwa muda mrefu ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Mradi huu unadhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya maendeleo, na jamii katika kuboresha elimu na ustawi wa watoto