Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemgomea mdhamini wa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, Robert Katula kutaka kujitoa kumdhamini Mbunge huyo katika kesi ya uchochezi inayomkabili mahakamani hapo.
Mdhamini huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba aliomba kujitoa kumdhamini Lissu kwa kile alichodai kuwa hana mawasiliano wala ushirikiano wowote na Mbunge huyo.
“Hatuna taarifa naye lakini pia ana ushirikiano wowote kwa kweli hivyo naomba kujitoa,” alidai Katula.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba alisema kuwa hawezi kujitoa kwa sababu mshtakiwa wake hayupo mahakamani kwa sasa na mahakama aina taarifa yoyote juu ya mshtakiwa huyo.
Alisema ni kweli kuwa rekodi ya mahakama ipo kimya juu mshtakiwa huyo hivyo ni jukumu la mdhamini kuwasilisha taarifa Mahakamani zitakazoeleza mahali alipo mshtakiwa.
“Tunaomba kuwapa tena muda wa kuweza kuwasilisha taarifa za mahali alipo mshtakiwa huyo, na niwaeleze tu kwamba hakuna namna ya nyie kujitoa kama mshtakiwa huyu hatofika mahakamani, mkijitoa nyie nani atakuwa na jukumu la kumleta hapa, “ aliwahoji wadhamini wa Lissu.
Naye mdhamini mwingine wa Lissu, Ibrahim Ahmed alidai kuwa wamefanya juhudi za kila aina kupata namba za simu ili kuweza kuwasiliana na Lissu awaeleze mahali alipo na maendeleo ya afya yake lakini wameshindwa.
“Tulifanya juhudi za kila aina kupata namba za simu ili kujua alipo lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa kuzipata namba hizo, ila bado naendelea kufanya juhudi zingine kwa lengo la kujua alipo, niiombe mahakama inipatie muda mwingine wa kufatilia jambo hili” alidai.
Awali Wakili wa Serikali Patrick Mwita alidai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa ila baadhi ya washtakiwa hawapo mahakamani hivyo wangependa kujua mahali walipo.
Hata hivyo baada ya wadhamini kueleza walipo washtakiwa wanaowadhamini, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 25, mwaka huu.
Kesi hiyo ilishafika katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini inashindwa kuendelea kutokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, ( Lissu )kuwa nchini Ubeljiji kwa ajili ya matibabu.
Lissu na wenzake watatu katika mahakama hiyo wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi katika gazeti la Mawio kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifaza uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
BREAKING: Taifa Stars na Mwakinyo wapo ndani ya Ikulu ya Rais Magufuli