Siku zimepita tangu sakata la Mwanamke mkazi wa Dar es salaam aitwae Asma kudai kuibiwa mtoto ambaye inadaiwa wakati akifanyiwa Ultra sound alikua na ujauzito wa Watoto mapacha lakini alipokwenda kujifungua aliambiwa amejifungua mtoto mmoja.
Baada ya kuwepo kwa mkanganyiko huo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameamua kuingilia kati kwa kuunda Tume ya Wataalamu mbalimbali kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuchunguza na kubaini ukweli.
“…baada ya kufuatilia hayo, nikiwa Waziri mwenye dhamana, nikiwa na wajibu wa kutenda haki nimeamua kuunda timu huru ya kuchunguza suala hili ambayo itaongozwa na Prof. Charles Majinge – daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama ambaye ndiye atakuwa Mwenyekiti.” – Ummy Mwalimu
Bi. Asma Juma mkaazi wa Mbande, DSM aliulalamikia uongozi wa Hospitali ya Temeke baada ya kudai kuibiwa mtoto baada ya kujifungua akisema alikuwa na ujauzito wa mapacha jambo ambalo lilipelekea Mganga Mkuu wa Mkoa Dr. Grace kuunda Tume kuchunguza ukweli ambapo ripoti ilisema kuwa Bi. Asma alikuwa na ujauzito wa mtoto mmoja lakini ripoti hiyo ilipingwa na familia.
“Mimi siwezi kutoka na kukukurupuka nikaongopa, nimeshajifungua Temeke hii si chini ya mara mbili sijawahi kuzusha hivyo, nimekwenda na vipimo vyangu na mwenye vipimo kakubali kwenye kikao ila Mganga mkuu tu anawabeba wale” – Asma Juma