Top Stories

Rais wa China avutiwa na Tanzanite na korosho, atuma ujumbe kwa JPM (+picha)

on

Rais wa China Xi Jinping afungua rasmi maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za nje na kuahidi kwamba Nchi yake itafungua milango zaidi kwa bidhaa za nje kuingia katika soko la China.

Katika hafla hiyo viongozi wa Mataifa 64 waliohudhuria akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mawaziri Wakuu wa Jamaica, Serbia na Greece. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa.

‪Aidha baada ya kufungua maonesho hayo Rais wa China ametembelea Mabanda ya nchi (5) yakiwemo mabanda ya Ufaransa, Ugiriki, Serbia, Jamaica na Tanzania.

Katika ziara ya kutembelea Banda la Tanzania Rais Xi Jinping alifuatana na Waziri Mkuu wa Jamaica; Greece na Serbia na kupokelewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa.

Balozi wa Tanzania Mbelwa Kairuki alitoa maelezo juu ya bidhaa mbalimbali za kilimo na madini zinazopatikana nchini Tanzania na vivutio vya utalii. Aidha, Balozi Kairuki aliwasilisha salaam za Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa Rais wa China.

Kwa upande wake Rais wa China ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje na ametuma salaam za pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China.

Aidha, Rais Xi alivutiwa zaidi na bidhaa ya korosho za Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo alitaka kufahamu zaidi juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la China.

Maonesho ya Kimataifa yataendelea hadi tarehe 10 Novemba 2019. Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho haya umeratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa ushirikiano na Ubalozi wa Tanzania China na umeshirikisha jumla ya Washiriki 20 kutoka sekta mbalimbali zikiwemo za bidhaa za kilimo, madini na utalii.

ZITTO KABWE KUHUSU UTEUZI WA CAG MPYA, ADAI NI WA KUFICHA WIZI, UFISADI

Soma na hizi

Tupia Comments