Klabu ya Yanga imewafungulia mashitaka wachezaji wake watatu waliovunja mikataba na timu hiyo kwa sababu tofauti .
Yanga katika Kesi hizo inadai fidia toka kwa wachezaji hao ambao kwa mujibu wa maeleezo ya klabu wamevunja mikataba na hivyo kukiuka makubaliano ya kisheria hali ambayo inalazimu sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya wachezaji hao .
Yanga imemfungulia kipa Juma Kaseja kesi ya kukiuka makubaliano ambapo imemuwekea kipa huyo kiwango cha fidia ya shilingi milioni 365,000,000/= ambayo atapaswa kulipa endapo atakutwa na hatia .
Kwa upande mwingine Yanga pia imefungulia mashitaka kama hayo mchezaji raia wa Uganda Emmanuel Okwi ambaye atapaswa kulipa fidia ya dola milioni moja endapo atakutwa na hatia .
Katika kesi hiyo pia yumo mshambuliaji wa Kibrazil Genilson Santos Santana maarufu kama Jaja ambaye ameburuzwa kortini baada ya kushindwa kurudi kuitumikia klabu hiyo baada ya mapumziko ya kumalizika kwa nusu ya mzunguko wa kwanza .
Jaja ambaye alishindwa kufanya vizuri kwenye mechi nane alizocheza hakurudi wakati wa kufanya hivyo ulipofika huku kukiwa na madai ya mchezaji huyo kupatwa na matatizo ya kifamilia .