Dakika kadhaa baada ya kushinda kesi dhidi ya Chadema Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alitoa nafasi kwa millardayo.com kuwa chombo pekee cha habari kumfanyia mahojiano. (Exclusive interview)
Yafuatayo ni maswali na majibu aliyoyatoa Zitto.
millardayo.com : Unadhani utakua na amani kuwa Chadema pamoja na haya yaliyotokea?
Zitto kabwe: ‘Kwanza nataka niseme wazi kabisa kwa Watanzania ambao ni Wanachama wa vyama vingine, wasio na vyama na kwa Wanachadema, ushindi huu sio ushindi dhidi ya Chadema, ni ushindi kwa Watanzania wote wanaopenda siasa safi, wanapenda taratibu za utawala bora zifatwe kwenye taasisi zetu, ni ushindi dhidi ya wanaotaka kukandamiza demokrasia ndani ya vyama, ni ushindi dhidi ya Wahafidhina wasiotaka mabadiliko katika vyama’
Huu sio ushindi dhidi ya chama kwa sababu siwezi kushindana na chama changu, ni chama ambacho kimenilea na nimekitumikia kwa muda wangu wote, zaidi ya nusu ya umri wangu ambao nimeishi…. kwa hiyo salamu ambazo napenda wananchi wazifahamu ni kwamba tunahitaji kuheshimu sana demokrasia na misingi ya haki za binadamu.
Naamini maamuzi ya Jaji John Utamwa yataweza kuweka utaratibu, watu ambao ni Wanachama wa vyama hawataonewa, hawatadhulumiwa wala kukandamizwa, watakua huru kutoa maoni yao pale wanapohitaji kufanya hivyo.
millardayo.com : Kilichotokea Mahakamani kitakufanya usiende kwenye ofisi za Chadema?
Zitto Kabwe: Hapana kwa sababu bado mimi ni Mwanachama wa CHADEMA, pamoja na kwamba katibu mkuu wa Chadema ametoa amri ya watu wasinipe ushirikiano lakini pale nitakapohitajika nitafanya shughuli za Chadema, nitafanya shughuli za nchi yangu.
Sasa hivi kuna maswala makubwa kuhusu katiba ya nchi yetu na ningependa Wananchi wajielekeze huko, sijafurahishwa sana na kinachoendelea hivi sasa manake Wananchi wameacha kujadili maswala ya msingi sana ambayo yanawahusu, nasikitika kuona vyombo vya habari ni habari za Zitto na Chadema, nashukuru jambo hili limekwisha sasa kwa muda huu.
Mimi niko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote wa CHADEMA ambae atakua tayari kufanya kazi na mimi kwa sababu naamini swala hapa ni ujenzi wa nchi yetu, ni ujenzi wa taifa letu na ninaamini hata kama nina mawazo kidogo lakini ninayo mawazo kwa ajili ya kuiendeleza nchi yetu.