Leo Jumanne, Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini imeanza kusikiliza kwa mara ya kwanza kesi ya kuamua iwapo itathibitisha kuondolewa madarakani kwa Rais Yoon Suk-yeol juu ya tamko lake la sheria ya kijeshi.
Lakini mwanasheria wa Yoon anasema kuwa Rais huyo hatohudhuria akitaja wasiwasi wa usalama wake.
Mahakama hiyo ilifungua kesi hiyo mwezi uliopita na ilimaliza mashauri ya awali ya kesi hiyo kabla ya hoja za ana kwa ana zilizopangwa leo Jumanne.
Mwanasheria huyo alisema timu ya pamoja ya uchunguzi inajaribu kutekeleza kibali cha kumkamata Rais kinyume cha sheria. Aliongeza kuwa Yoon atahudhuria kesi hiyo pale tu masuala kuhusiana na usalama wake yakiwa yametatuliwa.
Timu ya uchunguzi inataka kumkamata Yoon aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma za kupanga uasi kwa kutoa tamko la sheria ya kijeshi mwezi uliopita.
Mwanasheria wa Yoon inaripotiwa kuwa aliwaomba wachunguzi kuahirisha utekelezaji wa kibali hicho ili Rais ajikite katika kesi yake ya kuondolewa madarakani.