Kulingana na ripoti rasmi zaidi ya watu 2,000 wamefariki katika tetemeko kubwa la ardhi lililopiga magharibi mwa Afghanistan Jumamosi hii, Oktoba 7, na kusababisha uharibifu mkubwa.
Zaidi ya watu 9,200 wamejeruhiwa na karibu nyumba 1,300 kuharibiwa au kusombwa. Shughuli za uokoaji zinaendelea kutafuta manusura katika magofu ya vijiji vilivyoathirika.
Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 katika kipimo cha Richter, likifuatiwa na mitetemeko minane yenye nguvu baada ya tetemeko hilo, ni mojawapo ya matukio mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha miaka ishirini.
Jumapili hii, mmoja wa wasemaji wa serikali amesema kuwa zaidi ya watu 2,050 wamefariki katika vijiji 13, watu 9,240 wamejeruhiwa na kwamba timu kumi za uokoaji zimefika eneo la tukio.
Shughuli za uokoaji zinaendelea. Watu bado wamenasa kwenye vifusi katika vijiji vilivyoathiriwa zaidi, anaripoti mwandishi wetu wa kikanda, Sonia Ghezali.
Kutakuwa na makumi ya vijiji vilivyoharibiwa kabisa au kiasi. Mamlaka ya Taliban imetangaza leo Jumapili asubuhi kwamba waathiriwa walikuwa na uhitaji wa haraka wa chakula, maji, dawa na mahema.
Zaidi ya miili 200 imepelekwa hospitali katika mkoa huo, afisa wa mamlaka ya afya huko Herat amesema.