Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kwamba zaidi ya wafanyakazi 20 wa serikali kuu katika Wizara ya Ufanisi wa Serikali, DOGE wamejiuzulu.
Hatua hii inaonekana kama upinzani dhidi ya juhudi za Elon Musk za kupunguza ajira.
Mjasiriamali huyo bilionea anayeongoza wizara hiyo, inayojulikana kama DOGE, ana lengo la kupunguza matumizi ya serikali.
Ripoti ya Associated Press, AP, imesema kwamba wafanyakazi 21 wa DOGE waliojiuzulu ni pamoja na wahandisi na wanasayansi wa data.
Juzi Jumanne, wafanyakazi hao walituma barua kwa Mnadhimu Mkuu wa Ikulu, Susan Wiles, wakisema kuwa hatua za DOGE za kuwafuta kazi wataalamu wa kiufundi, kushughulikia vibaya taarifa nyeti, na kuharibu mifumo muhimu zinaenda kinyume na dhamira yao iliyotangazwa ya kuboresha teknolojia na programu za serikali kuu ili kuongeza ufanisi na uzalishaji wa serikali.
Inaripotiwa kuwa wafanyakazi hao 21 walikuwa na ujuzi wa hali ya juu katika kituo ambacho zamani kilijulikana kama Huduma ya Kidijitali ya Marekani.
Musk aliweka kwenye mitandao ya kijamii siku hiyo hiyo kwamba ripoti ya AP ni “habari potofu.” Alisema kwamba wale waliojiuzulu walikuwa “masalia wa siasa za Democrat” ambao wangefutwa kazi kama wasingejiuzulu.