Zaidi ya wahalifu 1,700 nchini Uingereza na Wales watatolewa gerezani mapema hii leo, kama sehemu ya mpango wa serikali ulioundwa kupunguza msongamano magerezani.
Hatua hiyo ilichochewa na serikali ya Labour iliyoingia madarakani siku chache baada ya uchaguzi mkuu mwezi Julai, lakini maafisa walikuwa tayari wameshalipangia wakati chama cha Conservative kikiwa bado madarakani.
Wafungwa 1,700 wanaopaswa kuachiliwa leo ni pamoja na 1,000 ambao kawaida huachiliwa ndani ya wiki moja.
Sera hiyo itawaruhusu wafungwa kuachiliwa baada ya kukamilisha 40% ya kifungo chao – badala ya 50% – katika jitihada za kuhakikisha vitanda 5,500 vinakuwa wazi.
Lakini sera hiyo haitatumika kwa wale waliopatikana na hatia ya makosa ya ngono, ugaidi, unyanyasaji wa nyumbani au baadhi ya makosa ya vurugu.