Mamlaka ya kitaifa ya magereza nchini Nigeria imethibitisha kwamba zaidi ya wafungwa 1,800 wametoroka jela nchini humo kufuatia shambulio la watu waliojihami kwa bunduki.
Washambuliaji hao waliripotiwa kuvamia gereza hilo lilipo katika mji wa Kusini Mashariki wa Owerri kwa kutumia vilipuzi.
Wafungwa sita wameripotiwa kurejea huku wengine 35 wakikataa kutoroka.
Polisi wanalaumu shambulio hilo lilifanywa na kundi linalotaka kujitenga la wenyeji wa Biafra, ambalo lilipigwa marufuku. Kundi hilo limeripotiwa kupinga madai hayo.
Mamlaka ya usimamizi wa magereza imethibitisha ni wafungwa 1,844 waliotoroka gerezani katika jimbo la Imo.
Watu waliokuwa wamejihami wa silaha nzito walivamia kituo cha kuwazuilia wafungwa mjini Owerri mapema jana Jumatatu, baada ya kuwasili wakiwa wamepanda gari aina ya pick up na mabasi, maafisa walisema.
Msemaji wa polisi alisema washambuliaji hao walitumia maroketi, maguruneti na silaha nyingine katika uvamizi huo.