RAIS Donald Trump ameamuru maafisa wa Marekani kuanza kutekeleza mpango wa kurudisha wahamiaji wasiokuwa na hati za kisheria, kama sehemu ya juhudi za kupambana na kile alichokiita “uvamizi” kwenye mpaka wa kusini.
Hatua hii inakuja huku Marekani ikituma wanajeshi 1,500 zaidi na kupanua mchakato wa kufukuza watu wasio na kibali walioingia nchini humo.
Trump pia alisitisha usafiri na kutowapa vibali wakimbizi, akisema, “Marekani haiwezi kubeba idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi.”
Uamuzi huu umewaacha maelfu ya watu wakiwa wamekwama wakingojea kuingia Marekani, ikiwa ni pamoja na zaidi ya 1,600 Waafghanistan ambao walithibitishwa kuingia lakini mipango yao imeshindwa kutekelezwa.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Caroline Leavitt, amesema Rais Trump ameshatuma taarifa hizi kwa mataifa mengine.
Hivi karibuni,Rais Trump alisaini amri za uhamiaji na mipango ya kuhusiana na mipaka, lengo likiwa ni kusitisha wahamiaji nchini Marekani.
Taarifa rasmi imesema sera ya kuondoa watu kwa haraka ilianza kutumika usiku wa tarehe 21 Januari, ikiwa na lengo la kuondoa wahamiaji wasiokuwa na hati za kisheria waliokamatwa ndani ya maili 100 (160 km) kutoka mipaka ya kimataifa.