Hadi sasa watoto 21,000 wanakadiriwa kupotea katika machafuko ya vita huko Gaza, wengi wao wakiwa wamekwama chini ya vifusi, wakizuiliwa, kuzikwa kwenye makaburi yasiyojulikana, au kupotea kutoka kwa familia zao, kulingana na shirika la Save the Children.
Vikundi vya ulinzi wa watoto vya shirika hilo vinaripoti kwamba uhamishaji wa hivi punde uliosababishwa na shambulizi huko Rafah umewatenganisha watoto zaidi na kuongeza zaidi mzigo kwa familia na jamii zinazowatunza.
Ni karibu haiwezekani kukusanya na kuthibitisha habari chini ya hali ya sasa ya Gaza, lakini angalau watoto 17,000 wanaaminika kuwa bila kusindikizwa na kutengwa na takriban watoto 4,000 wana uwezekano wa kupotea chini ya vifusi , na idadi isiyojulikana pia katika makaburi ya pamoja.
Wengine ‘wametoweka’ kwa nguvu, ikiwa ni pamoja na idadi isiyojulikana iliyozuiliwa na kuhamishwa kutoka Gaza, mahali walipo haijulikani na familia zao huku kukiwa na ripoti za kutendewa vibaya na kuteswa.
Wakati huo huo, timu za ulinzi wa watoto za shirika hilo la usaidizi zinaonya juu ya hatua za haraka zinazohitajika kulinda watoto waliotenganishwa na wasio na walezi – hatua ambayo inadhoofishwa sana na kuzorota kwa hali ya usalama.