Takriban watu 63 wameuawa na zaidi ya 40 wakiachwa na majeraha kufuatia moto kwenye jengo la ghorofa nyingi katikati mwa jiji la Johannesburg, Afrika Kusini, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani na mfanyakazi wa dharura.
Msemaji wa huduma za dharura za Johannesburg Robert Mulaudzi amesema moto huo uliotokea Alhamisi asubuhi uliteketeza jengo lililoko katikati mwa jiji la kibiashara, na idadi ya waliofariki inaendelea kuongezeka huku miili 63 ikipatikana kutoka eneo hilo kufikia sasa tunapochapisha taarifa hii.
Inaelezwa kuwa angalau mtoto mmoja alikuwa miongoni mwa waliofariki, na wale waliojeruhiwa katika moto huo wanapokea matibabu katika vituo mbalimbali vya afya.
Mulaudzi alisema jengo hilo lilikuwa “makazi yasiyo rasmi” ambapo watu wasio na makazi wamehamia kutafuta makao bila makubaliano yoyote rasmi ya kukodisha. Alisema hilo lilifanya iwe vigumu kwa waokoaji kupekua jengo hilo.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya mtandaoni ya News24 ya Afrika Kusini.