Wafanyakazi wa huduma za uokoaji Zambia wameendelea kuwatafuta wachimba madini wasiopungau 25 waliofukiwa na maporomoko ya udongo wakiwa hai katika mgodi wa madini ya shaba. Haya yameelezwa na Waziri wa Madini wa Zambia, Paul Kabuswe.
Serikali imesema kuwa wachimba madini hao 25 katika mgodi wa Seseli umbali wa kilomita 400 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Lusaka walifunikwa na maporomoko ya udongo Alhamisi iliyopita usiku ambapo mvua kubwa zimesabisha maji kujaa mgodini.
Zoezi la uokoaji lilianza Ijumaa na huku ikiwa haijulikani ni wachimba madini wangapi ambao wamefunikwa na maporomoko ya udongo hadi sasa, Waziri wa Madini wa Zambia ameeleza kuwa hadi sasa familia 25 zimedai kupoteza ndugu zao waliokuwa wakifanya kazi katika mgodi huo wakati maafa yalipotokea.
Wafanyakazi wa uokoaji wakiwemo wanajeshi na wafanyakazi wengine kutoka makampuni makubwa wamekuwa wakichukua tahadhari katika zoezi la uokoaji kutokana na udongo kujaa maji; jambo lililopunguza kasi ya oparesheni.
Jana Jumatatu mfanyakazi mmoja wa kitengo cha uokozi alisema kuna matumaini ya kuwapata wachimba mgodi wakiwa hai. Zambia ni kati ya nchi 10 wazalishaji wakuu wa shaba duniani. Chingola, mji unaopatikana katika Ukanda wa Shaba una migodi mikubwa ya shaba yenye mashimo ya wazi yaliyozungukwa na rundo kubwa la taka za mawe na ardhi ambazo zimechimbwa nje ya migodi hiyo.