Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambae pia ni mlezi wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Tanga Mhe. Hemed Sulaiman Abdullah amewataka viongozi wa chama na serikali kuhakikisha wanasimama katika muelekea mmoja wa kupinga vitendo vya ukatili katika maeneo yao.
Mhe Sulaiman Ameyabainisha hayo mkoani Tanga wakati akizungumza na viongozi mbalimbali mkoani humo mara baada ya kuwasili tayari kwa kuanza ziara yake ya siku nne mkoani Tanga ya kukagua miradi ya maendelea na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua Tanga kiuchumi kwa kuleta miradi ya kimkakati ikiwemo maboresho ya bandari ya Tanga.
Nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga amewataka wakandarasi waliopata dhamana ya kutekeleza miradi mbalimbali mkoani tanga kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati kwa manufaa ya wananchi.