Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema uvamizi wa wanajeshi wake katika eneo la Kursk nchini Urusi ni sehemu ya “mpango wa ushindi” ambao atauwasilisha kwa Rais wa Marekani Joe Biden mwezi ujao.
Akizungumza katika kongamano siku ya Jumanne, Rais Zelensky alisema mafanikio ya mpango huo yatategemea Rais Biden na iwapo Marekani itaipa Ukraine “kile kilicho katika mpango huu au la, [na] ikiwa tutakuwa huru kutumia mpango huu, au la”.
“Inaweza kuonekana kuwa kubwa sana kwa baadhi, lakini ni mpango muhimu kwetu,” aliongeza, akisema kwamba ataonyesha mpango huo kwa wagombea urais wa Marekani Kamala Harris na Donald Trump.
Idadi ya wanajeshi wa Ukraine walifanya uvamizi katika eneo la Kursk la Urusi mapema mwezi wa Agosti, na Urusi hadi sasa inaonekana imeshindwa kuwazuia.
Rais Zelensky pia alifichua kuwa Ukraine hivi majuzi ilifanya jaribio la kwanza la mafanikio la kombora la balestiki lililotengenezwa nchini.
Aliipongeza sekta ya ulinzi ya nchi yake, lakini alikataa kueleza maelezo zaidi kuhusu kombora hilo.