Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amekiri kupiga hatua kuelekea kupata dhamana ya usalama kuhusiana na makubaliano ya madini na Marekani.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa nchi hizo mbili zimefikia makubaliano mapana kuhusu maendeleo ya pamoja ya rasilimali ya madini ya Ukraine.
Rasimu ya mwisho ya makubaliano hayo inajumuisha sentensi inayosema, “Serikali ya Marekani inaunga mkono juhudi za Ukraine za kupata dhamana ya usalama inayohitajika ili kuleta amani ya kudumu.”
Akizungumza na wanahabari jana Jumatano, Zelenskyy alieleza kuwa amefurahia toleo la mwisho la makubaliano hayo. Ukraine imekuwa ikishinikiza kuhakikishiwa usalama kutoka kwa Marekani ili kuzuia mashambulizi ya baadaye ya Urusi.
Zelenskyy pia alisema ni muhimu kwa nchi yake kutokuwa na madeni.
Ripoti za vyombo vya habari zilisema Marekani ilidai haki kwa baadhi ya mapato makubwa yanayoweza kupatikana kutoka kwenye rasilimali ya madini ya Ukraine, lakini Zelenskyy alisema kuwa rasimu hiyo haijataja madai hayo.
Aidha, Zelenskyy alirejelea kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba atazuru Marekani kesho Ijumaa. Alisema kuwa kukutana na Trump kabla ya mazungumzo kati ya Trump na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ni ishara muhimu.
Trump alisema katika mkutano wa Baraza la Mawaziri jana Jumatano kwamba Zelenskyy atawasili Marekani kesho Ijumaa kusaini makubaliano, na kuyaita kuwa “makubaliano makubwa sana.