Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anatarajiwa kutembelea jijini Washington nchini Marekani wiki hii kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Donald Trump, bila shaka ni juhudi za kufanikisha amani ya haki.
Ijumaa iliyopita Trump alisema anatarajia kukutana na Zelenskyy wiki hii ikiwa ni mapema zaidi.
Siku iliyofuata, Zelenskyy kupitia ujumbe wa video, alisema: “Tunaandaa ratiba ya wazi ya mikutano na washirika wetu muhimu: Marekani, Ulaya na dunia ya Kiislam. Tuna tarehe mahsusi.”
Zelenskyy pia anatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Usalama wa Munich, utakaoanza nchini Ujerumani Ijumaa wiki hii, na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na viongozi wa Ulaya kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Ukraine, Andriy Yermak, ameliambia shirika la habari la AP Alhamisi iliyopita kuwa mjumbe maalum wa Marekani nchini Ukraine na Urusi, Keith Kellogg atakwenda Ukraine mwishoni mwa Februari.