Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliwasili Marekani siku ya Jumapili kuwasilisha mpango wake wa vita kwa Rais Joe Biden, pamoja na wagombea urais Donald Trump na Kamala Harris, huku Marekani ikiendelea kupinga matumizi ya Ukraine ya silaha za NATO kwenye malengo ndani ya ardhi ya Urusi. Huku mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi yakionekana kukwama, Zelensky anatazamiwa kuwasilisha mapendekezo yake ya mpango wa kufikia “amani ya haki na utulivu”, ambayo anatumai kuwa tayari ifikapo Novemba.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Jumapili aliwasili Marekani kwa ziara muhimu ya kuwasilisha mpango wa Kyiv wa kumaliza miaka miwili na nusu ya vita na Urusi.
Zelensky atawasilisha mapendekezo yake — ambayo anayaita “mpango wa ushindi” — kwa Rais Joe Biden, pamoja na wawaniaji urais Kamala Harris na Donald Trump.
Ziara hiyo inakuja baada ya majira ya mapigano makali: huku Moscow ikisonga mbele kwa kasi mashariki mwa Ukraine na Kyiv ikiendelea kushikilia eneo la Kursk nchini Urusi.
Pia inakuja wakati Kyiv kwa wiki imeishinikiza Magharibi kuiruhusu kutumia silaha za masafa marefu kushambulia shabaha ndani ya Urusi — hadi sasa haijafaulu.
Watakapokutana katika Ikulu ya White House siku ya Alhamisi, Zelensky anatarajiwa kujaribu kumshawishi Biden kubadili mawazo yake.