millardayo.com ilifika kwenye moja ya sehemu zilizodaiwa kukumbwa na kashikashi ya kundi la Panya Road Dar es salaam January 2 2015 iitwayo Plaza Catalunya ambako Mtangazaji Ephraim Kibonde na wateja wengine walilazimika kulala chini.
Mkurugenzi wa Catalunya Mr. Atik ameiambia millardayo.com >>> ‘Kuhusu kadhia ya hawa Panya Road niliona watu wanakimbia wakitokea Mlimani City, Sinza A na Meeda ambapo Wateja wetu walikua wamerelax wanasikiliza mziki lakini walivyoona watu wanakimbia wakapaniki na wakaanza kukimbia’
‘Hakuna uharibifu wowote uliotokea Catalunya wala gari la mteja lililovunjwa ila Wateja tu wameumia kidogo kwa kukatwa na vyupa na glasi kutokana na zile purukushani za watu kulala chini kujificha ila hakuna aliejeruhiwa na kundi la Panya Road’ – Mr. Atik
Usiku wa January 2 2014 Kamanda wa polisi Suleiman Kova wa kanda maalum ya Dar es salaam aliwatoa hofu wananchi kupitia TBC 1 kwa kusema kweli kumekua na uhalifu mtaani lakini sio kwa kiasi hicho kama ilivyotangazwa, yaani uvumi ulikua mkubwa kuliko ukweli wenyewe wa tukio.
Alisema pia kilichotokea ni kundi hili la vijana waliokosa kazi kuanzisha vuguvugu la kulipiza kisasi baada ya mwizi mwenzao kuuwawa.
Baadhi ya watu maarufu walioongea na millardayo.com na kuthibitisha vijana hawa kusogelea mitaa yao ni pamoja na rapper Izzo Bizness ambae alisema waliingia kwenye mtaa wao Sinza ila wakakimbia muda mfupi baadae baada ya jirani yao kufyetua risasi hewani.
Mwimbaji Peter Msechu alisema aligeuza na kukatisha safari ya kwenda kununua umeme baada ya kushuhudia watu wakikimbia wakitokea upande anaoelekea, baadae vijana hao walimvamia jirani wa Msechu aliekua nje na kumchana sikio baada ya purukushani za kuivuta hereni yake.
Mwimbaji Ray C aliandika kwenye page yake ya instagram ‘Sina hamu na hawa panya road, jana nilikuwa sehemu flani sinza nakula kitimoto nilivyoona watu wanakimbia nikatoka nduki bila viatu nikaingia kwenye gari mbio mara mbele yangu nikakutana na lundo la watu wakinoa mapanga barabarani, niligeuza gari utafikiri niko kwenye movie nikajikuta nimefika osterbay polisi bila viatu mpaka askari wakanicheka‘
‘Serikali tunaomba mkamate hawa vijana kwakweli maana tumezoea amani sasa mambo kama haya yakitokea yanakosesha amani kabisa kwa wananchi!Na uhakika Jeshi la polisi litafanya kazi yake yani nilijihisi kama niko Rwanda maana nakumbuka mapanga yale niliwahi yaona kwenye muvi ya Somewhere in April na Hotel Rwanda!!!‘
Kwa kumalizia Ray C akaandika ‘Sasa wale waliosema bora damu imwagike nadhani kauli itabadilika maana kama Panya Road wanatupelekesha hivi je hiyo Vita!!!, Je hiyo vita, si tutapanda juu ya nyumba zetu!!!!! Jamani msicheze na haya mambo jamani, amani ndio sifa kuu ya nchi yetu……..Eeh Mungu tuepushe na haya mambo‘
Hii sauti hapa chini ni ya mtangazaji Ephraim Kibonde January 2 2014 ambae alikumbwa na kadhia hiyo Catalunya na kuamua kurudi studio ili kusaidia Wananchi taarifa.