NIPASHE
Wanachama wa CCM Zanzibar wamesema hawapo tayari kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kitendo cha kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Katibu wa Mkoa wa Mjini CCM, Muhammed Nyawenga amesema Lowassa asidhani kuwa wanachama wengi wa CCM walimuunga mkono wakati alipotangaza nia ya kugombea Urais wa Muungano kupitia chama hicho, akadhani kuwa na sasa watakuwa pamoja naye.
“Tunamwambia Lowassa kama mvuvi wa pweza basi tutakutana mwambani”– Muhammed Nyawenga.
Nyawenga amesema uamuzi wa Lowassa kutoka CCM sio jambo la kukishtua chama, wanachama wala viongozi wa chama hicho na kamwe CCM haiwezi kudhoofika wala kupasuka kwani sio mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na kiongozi muandamizi na kujiunga na upinzani.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa mjini Magharibi ambae alikuwa kinara katika kumuunga mkono Lowassa wakati akiomba ridhaa ya Chama hicho kugombea Urais kupitia CCM, Borafya Silima Juma amesema kiongozi huyo anapenda madaraka na ukubwa na ndio maana baada ya jina lake kutopita ameamua kujiunga na CHADEMA.
NIPASHE
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi imemhoji Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa madai ya kukutwa na fedha zinazodaiwa za kuwapa Wajumbe ili wamchague katika kura za maoni.
Nape alikamatwa wakati akitoka ndani ya Benki na alipofika nje alikutana na askari wa kikosi hicho na kumuweka chini ya ulinzi.
Maofisa hao walimchukua kwa mahojiano ofisi ya TAKUKURU yaliyochukua saa tano, kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri na kuachiwa.
Waandishi wa habari waliokuwepo eneo hilo, walishuhudia askari hao wakimkamata na Nape kujaribu kupinga.
“Mheshimiwa sisi ni askari wa TAKUKURU , usijivunjie heshima tunakuomba uongozane na sisi kuelekea ofisini kwetu,” alisema mmoja wa askari hao.
Waandishi wa habari walipomhoji Nape kuhusu tuhuma hizo, alikiri kwenda ofisi hizo, lakini alikataa kueleza alichoitiwa na kudai alikwenda kwa ajili ya matembezi yake binafsi.
“Mimi sikuhojiwa na Takukuru ila nilikwenda kwa matembezi yangu binafsi,” alisema Nape.
Kamanda wa Taasisi hiyo, Stephen Chami alipotakiwa kuthibitisha tuhuma hizo, aliwataka waandishi wafanye subira kwani wapo katika mahojiano nae, baada saa nne kupita, alipigiwa tena simu na kukiri kumhoji Nape, katika mahojiano hayo Nape alisema fedha hizo alizichukua kwa ajili ya kuwalipa Mawakala.
Nape ametangaza nia ya kugombea jimbo la Mtama mkoani Lindi ambalo kwa sasa linashikiliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
HABARI LEO
Wanachama wa CCM na Chadema wa familia mbili tofauti wamepigana na kuumizana vibaya wakizozana kuhama katika vyama hivyo.
Mkasa huo ulitokea juzi katika Kijiji cha Nondo Wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa baada ya Wagombea Udiwani wa CCM kumaliza kikao chao, wakiwaomba wanachama wenzao wawachague katika kura ya maoni.
Ugomvi huo ulihusisha familia ya Katibu Mwenezi wa CCM wa kata hiyo, Meidi Sinkamba na mwanawe Hamoud Milambo na familia ya mwanachama wa CHADEMA, Waton Silawe na mwanawe Megji Silawe.
Ilidaiwa kuwa Megji alianza kumshambulia kwa maneno Katibu huyo Mwenezi wa CCM akihoji kwa nini amewaleta madiwani hao wa CCM kujinadi kijijini kwao wakati wanachama wa CHADEMA wakifurahia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiunga rasmi na chama hicho.
Malumbano hayo ya maneno yalimkasirisha Hamoud ambaye aliingilia kati ili kumsaidia mama yake mzazi huku Mzee Kasomo naye akimtetea mwanawe Megji.
MTANZANIA
Wanafunzi wa Shule za Msingi Kisiwa kilichopo Ukerewe Mwanza wanasoma kwa zamu kutokana na ukosefu wa madarasa.
“Hali ya Wanafunzi kupata elimu ni jambo la msingi lakini miundombinu hairidhishi, shule yetu ina majengo mawili yenye vyumba vine vya madarasa, wanafunzi wanasoma kwa zamu”—Mwenyekiti wa Kitongoji, Muzumari Kasanzila.
Mwenyekiti huyo amesema Diwani wa Kata yao amehamia Morogoro na Mbunge Salvatory Machemuli hajafika muda mrefu kisiwani hapo hivyo hajui matatizo ya Wananchi wake.
HABARI LEO
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajab Luhavi amesema hakuna utaratibu wa kikanuni wa kumzungumzia mwanachama anayekihama chama hicho na kuwa wanajiandaa na siasa za kiushindani ili kulinda hadhi na heshima ya CCM.
Naibu Katibu Mkuu huyo amemtakia kila la heri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyehamia CHADEMA.
Luhavi amesema suala la kuzungumzia mwanachama anayehama limekuwa la mazoea tu, na siyo la kikanuni rasmi na kwamba mara nyingi wanapoondoka hawasemi, bali huzungumza wanaporejea katika chama hicho.
“Kikubwa wanaoondoka leo, kesho wanarudi wanasema mtusamehe sana, tulikasirika ndio maana tuliondoka, na leo tumerudi nyumbani”– Rajab Luhavi.
MTANZANIA
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya NEC amesema wanapinga kauli ya ushindi wa bao la mkono iliyotolewa na Nape Nnauye, na kukanusha uvumi ulioenea kwamba wanataka kuchakachua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.
“Tunasikitishwa na matamshi kama haya ya bao la mkono na mengineyo, nawasihi wanasiasa na Viongozi kuepuka kauli za aina hii kwa sababu wakati mwingine matamshi yanatafsiriwa tofauti”— Jaji Damian Lubuva.
Wakati huohuo Tume hiyo imesema zoezi la Wagombea Urais kuchukua Fomu linaanza leo ambapo Fomu hizo zinatolewa bure ila zitakaporudisha Wagombea watatakiwa kulipia dhamana ya Milioni moja.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos