Mlipuko wa radi kwenye kanisa moja nchini Uganda uliua takriban watu 14 na kuwajeruhi 34 walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya maombi Jumamosi, polisi walisema
Tukio hilo lilitokea katika kambi ya wakimbizi ya Palabek wilayani Lamwo kaskazini mwa Uganda, polisi walisema kwenye chapisho kwenye jukwaa la X siku ya Jumapili.
“Waathiriwa walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya maombi wakati mvua ilianza kunyesha mwendo wa saa kumi na moja jioni, na radi ilipiga saa kumi na moja unusu,” polisi walisema.
Polisi hawakutambua uraia wa waathiriwa lakini kambi hiyo na zingine katika eneo hilo zinahifadhi wakimbizi kutoka Sudan Kusini.
Wengi wa wakimbizi hao walikuwa wamekimbia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha umwagaji damu vilivyoikumba nchi hiyo muda mfupi baada ya uhuru wake mwaka 2011.
Wahasiriwa wengi walikuwa vijana na ni pamoja na msichana wa miaka tisa, polisi walisema.
Dhoruba mbaya za radi ni za kawaida katika nchi hiyo ya Afrika mashariki, haswa katika majengo ya shule ambapo mara nyingi yanakosa vikondakta vya kudhibiti radi.