Shirikisho la kupambana na unene wa mwili wa kupindukia duniani, (World Obesity Federation ), limetahadharisha kuwa zaidi ya nusu ya watu duniani watakuwa na uzito wa mwili mkubwa kupitiliza kufikia mwaka 2035.
Watu zaidi ya bilioni nne wataathiriwa, huku viwango vikitarajiwa kuongezeka kwa kasi zaidi miongoni mwa watoto, imesema ripoti.
Nchi zenye kipato cha chini na cha kati barani Afrika na Asia zinatarajiwa kushuhudia ongezeko kubwa zaidi la watu weney uzito wa mwili wa kupindukia.
Ripoti inabashiri kuwa gharama ya unene wa mwili wa kupindukia itapanda na kufikiza zaidi ya dola trilioni 4 za Kimarekani (£3.3tn) kila mwaka ifikapo 2035.
Ripoti hiyo imeelezea hasa kuongezeka kwa viwango vya uzito wa mwili miongoni mwa watoto na vijana wadogo wenye umri wa chini ya 18, huku viwango vyao vikitarajiwa kuongezeka mara dufu ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2020 miongoni mwa wavulana na wasichana.
Ripoti za mwaka 2016 zilibashiri kuwa huenda mwaka 2025 ndio ungekuwa mwaka wenye watu wenye uzito mkubwa kupitiliza duniani.
Marekani na Uchina ndio zilikuwa miongoni mwa nchi zenye watu walio na uzito kupindukia, Uingereza ikiongoza mataifa ya Ulaya. Japan ndilo taifa tajiri ambalo lina watu wachache walio na uzito wa kupindukia.