Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza kuwa changamoto ya upungufu wa umeme pamoja na umeme mdogo (low voltage) Jijini Tanga kumalizika Machi 2023.
Hayo yamebainishwa Oktoba 25, 2022 Jijini Tanga katika kikao kazi kati ya TANESCO na wateja kulifanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort.
Awali akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Tanga mjini, Mhe. Hashim Mgandilwa alisema Dunia inapitia katika changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanayopelekea kuwa na uhaba wa maji katika vyanzo vya kufua umeme.
“Ndugu zangu, mmoja wa wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi ni taasisi yetu ya TANESCO, tunachangamoto ya maji katika mito ambayo inapeleka maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme “, alisema Mhe. Mgandilwa.
Akielezea hatua ambazo TANESCO inazichukua kukabiliana na changamoto za umeme Jijini Tanga, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji Umeme, Mha. Abubakari Issa alisema ni pamoja na uboreshaji wa njia za kusafirisha umeme.
“Katika kuboresha njia ya kusafirisha umeme kutoka Ubungo kupitia Chalinze hadi Tanga, kipande cha Dar es Salaam hadi Chalinze kimekamilika”, alisema Mha. Issa.
Aliongeza kuwa, njia ya umeme ya sasa inapitisha megawati 75 na uboreshaji utakapokamilika itakuwa na uwezo wa megawati 150 hadi 170.
Aidha, aliwahakikisha wafanyabiashara wakubwa hali ya upatikanaji wa umeme Jijini Tanga kuimarika zaidi ifikapo Machi 2023.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja, Bw. Martin Mwambene alisema hivi sasa shirika linaelekea kuwekeza katika vyanzo mchanganyiko vya kuzalisha umeme.
“Tunakamilisha masuala ya manunuzi na mwisho wa mwaka huu, tunatarajia kuanza mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya jua Kishapu Shinyanga” alisisitiza Bw. Mwambene.