Mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere amesema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Fimbo nyeupe duniani ambayo kitaifa yatafanyika Mkoa wa Manyara.
Maadhimisho ya siku ya Fimbo nyeupe (watu wasioona) yatafanyika October 21 mwaka huu kitaifa mjini Babati ambapo zaidi ya watu 700 wenye ulemavu wa macho(watu wasioona) wanatarajia kushiriki maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa chama cha watu wasioona nchini Omar Sultan amesema walemavu wengi wa macho nchini wanashindwa kuwa na fimbo nyeupe kutokana na kushindwa kumudu gharama huku akiiomba Serikali kusaidia kupunguza gharama ili kuwawezesha walemavu wa macho kuwa na fimbo hizo kwaajili ya kuwasaidia kujongea.
Kauli mbiu ya Maadhimisho haya inasema “Wasioona tujumuishwe katika ajira,michezo na teknolojia ya habari na mawasiliano kwa maendeleo endelevu nchini”